Rais Samia awaapisha Mwenyekiti na Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewaapisha Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele na Mjumbe wa Tume hiyo Jaji Mwanaisha Athuman Kwariko baada ya kuwateua kushika nyadhifa hizo tarehe 27 Desemba mwaka 2022.
Rais Samia amewaapisha viongozi hao wa Tume katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino Mkoa wa Dodoma ambapo katika hafla hiyo pia amewaapisha Mawaziri, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Mkuu na viongozi wengine aliowateua hivi karibuni.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia amewatakia viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi utekelezaji mwema wa majukumu yao.
Mwenyekiti Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo alikuwa Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na nafasi yake imechukuliwa na Jaji Mwanaisha Kwariko.
Baada ya kuapishwa, Mwenyekiti Jaji Mwambegele aliwasili Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi zilizopo Njedengwa jijini Dodoma na kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake Jaji Mst. wa Mahakama ya Rufaa Semistocles Kaijage ambaye amestaafu.